728x90 AdSpace

  • Latest News

    Saturday, 8 October 2016

    Jali afya yako, matibabu ya figo gharama kubwa, hayana uhakika


    Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa mwaka 2011, asilimia 70 ya watu wanaoishi  kusini mwa Jangwa la Sahara ikiwamo Tanzania, idadi kubwa watakuwa wameathirika na maambukizo ya figo ifikapo mwaka 2023.
    Utafiti huo ulionyesha kuwapo kwa kati ya asilimia nane mpaka 16 ya waathirika wa figo duniani. Utafiti huo unaibainisha Tanzania kwenye nafasi ya 54 katika nchi zilizoongoza kwa vifo vinavyotokana na ugonjwa huo na asilimia 1.03 ya wananchi wake hufariki kila mwaka.
    Wakati utafiti wa WHO ukieleza hivyo imeelezwa kuwa kudharau magonjwa mbalimbali ikiwamo kisukari, shinikizo la damu na uzito mkubwa kunachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la maradhi ya figo.

    Licha ya maradhi hayo kuwa na gharama kubwa ya matibabu bado watu hawaoni haja ya kupima afya zao mara kwa mara na kutibu magonjwa yanayochangia uharibifu wa figo ama kwa makusudi au kwa kutokufahamu.
    Daktari bingwa wa magonjwa ya figo wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Onesmo Kisanga anasema kuna sababu nyingi zinazochangia kuharibika kwa figo. Anasema kisukari kinaongoza kwenye orodha hiyo na mgonjwa anahitaji kuwa makini kufuata masharti ili kujiepusha.
    “Wapo wenye kisukari ambacho hakijaanza kuwaletea madhara, hawa wapo kweney hatari zaidi ya kuharibu figo. Iwapo utaratibu wa kupima afya mara kwa mara utafuatwa ni rahisi kuepuka kwa kutambua kisukari hivyo kujilinda na maambukizo ya figo pia,” anasema Dk Kisanga.
    Alisema maradhi mengine yanayochangia kuharibu figo ni shinikizo la damu na uzito mkubwa. “Kutokana na wananchi kupuuzia suala la kuangalia  afya zao, hugundulika na maradhi yote kwa wakati mmoja,” anaeleza rais huyo wa chama cha madaktari wa figo.
    Anashauri kufanya vipimo vya afya kila mara, kupata ushauri wa madaktari na kuepuka yale wanayoshauri wataalamu wa afya ikiwamo kupunguza uzito, kula vyakula vinavyoshauriwa ili kujiepusha na maradhi hayo.
    Anasema licha ya maumivu kwa mgonjwa lakini hautibiki kirahisi na gharama za matibabu yake ni kubwa na wengi wanashindwa kuzimudu.
    Wataalamu wa afya wanasema matumizi mabaya ya dawa hasa za maumivu, zile za kienyeji na baadhi ya dawa za Kichina ni miongoni mwa vitu vinavyopaswa kuepukwa ili kujiweka salama. Vingine ni uvutaji wa sigara na  unywaji wa pombe kupita kiasi.
    Kuhusu matibabu, Dk Kisanga anasema usafishaji wa figo huhusisha utoaji wa maji yaliyojaa mwilini, uchafu na sumu za vyakula au dawa. Anasema tiba hiyo hugharimu Sh300,000 na mgonjwa hutakiwa kufanyiwa walau mara tatu kwa wiki.
    “Huduma hii inatolewa Muhimbili katika Kitengo cha Renal Dialysis Unity. Akishaanza, mgonjwa anatakiwa kutibiwa kwa  maisha yake yote,” anasema Dk Kisanga.
    Anafafanua kuwa tiba hiyo husaidia kuondoa maji yasiyohitajika mwilini baada ya figo kushindwa kufanya kazi na taka zilizomo kwenye damu. Kwa kawaida figo huchuja uchafu.
    Dk Kisanga anasema, usafishaji wa figo hufanywa kwa  wagonjwa ambao  figo zao zimeathirika kwa kiasi kikubwa ambao hufungwa mipira maalumu na kuunganishwa na mashine yenye figo bandia ambayo hufanya kazi iliyokusudiwa.
    “Mgonjwa hulala akifanyiwa tiba hii kwa saa nne, bila kuchomwa sindano ya usingizi, kwa kuwa haina maumivu makali. Vilevile mgonjwa hutobolewa eneo maalumu mwilini kwa ajili ya kupitishia mipira. Kuna wanaotobolewa shingoni au mkononi kulingana na anavyotaka mgonjwa,” anasema Dk Kisanga.
    Anaongeza kuwa pamoja na tiba hiyo kuwa ghali bado ina uhakika wa kutibu kwa asilimia 40 hadi 50 pekee. Tiba nyingine ambayo mgonjwa anaweza kupewa ni kupandikiza figo ambayo kwa sasa haifanyiki nchini.
    Akizungumzia upatikanaji wa tiba hiyo, Mkurugenzi wa MNH, Profesa Lawrence Museru anasema kuanzia Januari mwakani itakuwepo hospitalini hapo na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaosafirishwa nje ya nchi kufuata matibabu hayo.
    “Kuna wagonjwa zaidi ya 120 wanaosafishwa figo kila siku ingawa zaidi ya asilimia 80 wanahitaji kupandikizwa. Huduma za nje ya nchi hugharimu kati ya Sh40 milioni na Sh60 milioni.
    Anafafanua kuwa Serikali inakusudia kuzijengea uwezo hospitali za Bugando, KCMC, Dodoma na Mbeya ili ziweze kupandikiza figo kutokana na ukubwa wa mahitaji yaliyopo.

    Kazi za  figo
    Binadamu ana figo mbili zenye maumbo yanayofanana. Zipo kwenye utando unaozunguka tumbo, chini kidogo ya mbavu. Zinachuja sumu yoyote inayoingia kwenye damu,    zinasaidia kuhifadhi na kudhibiti kiwango cha maji na madini mwilini.
    Hutengeneza mkojo na kunyonya madini na kemikali muhimu na kuzirudisha katika mzunguko wa damu na   kutoa nje uchafu usiohitajika. Zinasaidia kutengeneza erythropoletin kiasili muhimu kwa utengenezaji wa chembechembe nyekundu za damu.
    Zinapokea asilimia 25 ya damu vilevile zinadhibiti na kurekebisha shinikizo la damu mwilini.

    Aina
    Dk Kisanga anasema zipo aina mbili za figo na kuzitaja kuwa ni figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla na muda mfupi au figo kushindwa kufanya kazi polepole na kwa muda mrefu.
    Daktari huyo anasema figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla na muda mfupi maana yake ni kwamba figo huharibiwa  taratibu na kuendelea kupunguza uwezo wake wa kufanya kazi kadiri siku zinavyokwenda.
    Dalili za aina hii ya ugonjwa huchelewa kujitokeza  na wakati  mwingine mwenye tatizo hajisikii chochote hadi anapougua ugonjwa mwingine na daktari kuhisi tatizo, ndipo hugundulika kuwa na tatizo hilo baada ya vipimo.
    Dk Kisanga anasema sababu za figo kushindwa kufanya kazi ghafla ni kupungua kwa mzunguko wa damu kwenye figo, kuwapo kwa kemikali mwilini au kushambuliwa na sumu.
    “Kushuka kwa kiwango cha  mzunguko wa damu humpata mtu anayetapika au anayeharisha na hanywi maji ya kutosha au anayepoteza damu nyingi mfano kutokana na ajali,” anasema Dk Kisanga.
    Anazitaja sababu nyingine kuwa ni ugonjwa wa moyo au moyo kushindwa kusukuma damu kwa ghafla. Anasema: “Tatizo hili pia humpata mtu ambaye ana bakteria kwenye damu ambao wanaweza kusababisha homa  au malaria.”
    Anazitaja sababu zinazofanya figo kufanya kazi taratibu lakini kwa muda mrefu na hatimaye kushindwa kabisa kuwa ni presha, kisukari, HIV, saratani na sumu mbalimbali zinazoingia mwilini.

    Dalili
    Dk Kisanga anasema dalili za kwanza ni kupungua kwa kiasi cha mkojo, kushindwa kupumua vizuri, kusikia kichefuchefu, kutapika na kuvimba miguu.
    Nyingine ni maji kujaa mwilini, matatizo ya moyo, ubongo, kukosa hamu ya kula na  kudhoofika  mwili. Kwa wasiogundulika haraka huvimba macho wakati wa asubuhi na uvimbe kupungua baadaye. Pia, huvimba miguu asubuhi na kupungukiwa damu.

    Kikwazo
    Upo uhaba wa madaktari wa figo nchini. Daktari bingwa wa figo wa  MNH, Jacqueline Shoo amesema licha ya changamoto ya gharama za matibabu kuna uhaba wa wataalamu pia.
    Anasema kuna madaktari bingwa watano MNH ambao hulazimika kuwahudumia wagonjwa wote wanaofika hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu.
    Ili kuwa salama wataalamu wa afya wanashauri kutodharau maradhi yanaweza kuwa chanzo cha kuua figo na kila ugonjwa utibiwe kwa wakati na wananchi wajali afya zao na kusaidia kukinga figo. 
    Source Mwananchi
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Jali afya yako, matibabu ya figo gharama kubwa, hayana uhakika Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top