Mapema mwezi huu, mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya chama cha Democratic, Hillary Clinton alilazimika kurekebisha ratiba yake baada ya afya yake kutetereka ghafla, hivyo kuhitaji huduma za kitabibu. Ni baada ya kushambuliwa na ugonjwa wa homa ya mapafu (pneumonia) unaoenezwa kwa njia ya hewa.
Taarifa za timu yake ya kampeni zilisema mgombea huyo alikuwa amechemka, hivyo kuongezewa maji na kupewa dawa na kushauriwa apumzike.
Daktari wake, Lisa Bardack alithibitisha hayo na kusisitiza kuwa Hillary anaendelea vizuri.
“Nilishauriwa nipumzike kwa siku tano lakini sikuzingatia ushauri huo. Nataka nimalizane na hili suala ili nirudi kwenye kampeni mapema iwezekanavyo,” alisema Hillary akikaririwa na gazeti moja.
Pneumonia hutokana na kuvimba kwa mkusanyiko wa seli katikam moja au mapafu yote mawili. Mara nyingi husababishwa na bakteria. Mwishoni mwa mirija ya kupumulia mwa mapafu yote, kuna mifuko midogo. Unapokuwa na homa ya mapafu, mifuko hiyo huvimba na kujaa maji na hivyo kusababisha ugumu katika kupumua, homa, kukohoa, kutoka jasho kutetemeka au kupoteza jamu ya kula.
Watu wa umri wowote huugua pneumonia, lakini ugonjwa huo huwakumba sana watoto na wazee wenye umri zaidi ya miaka 65
“Mwanangu aliwahi kuugua na tulilazwa hospitali. Sifahamu kama watu wazima nao wanaugua. Sijawahi kuona,” anasema Jackline Champanda .
Homa ya mapafu husababisha vifo vingi duniani.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa asilimia tano ya vifo vya watoto vilivyotokea mwaka 2008 vilisababishwa na pneumonia. Mwaka huo ugonjwa huo ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 675,000 duniani.
Katika kukabiliana na ugonjwa huo, Shirikisho la Kimataifa la Wafadhili wa Chanjo Duniani (Gavi) linatoa chanjo ya pneumonia (pneumococcal vaccines) kwa nchi zaidi ya 50 zinazoendelea. Tangu mwaka 2010, shirikisho hilo limetoa chanjo kwa zaidi ya watoto milioni 47 huku idadi ya watoto walionufaika kwa chanjo nyinginezo wakifika milioni 277 kuanzia mwaka 2011 mpaka 2015.
Gavi na WHO zinatoa chanjo hizo kwa wote wanaohitaji. Watoto hupata chanjo mara tatu; wakiwa na wiki nane tangu kuzaliwa, wiki 16 na ya mwisho wanapotimiza umri wa mwaka mmoja. Wazee na wenye magonjwa sugu hupewa mara moja na kuzuia kwa kiasi kikubwa uwezekano wa kupata tena maambukizi hayo.
Wengine ambao wako hatarini kupatwa na ugonjwa huo ni watumiaji wa dawa za kulevya.
Takwimu zinaonyesha watu wanane kati 1,000 nchini Marekani husumbuliwa na maambukizi haya ambayo hutokea zaidi wakati wa kipindi cha baridi kali.
Wataalamu
Mtaalamu wa magonjwa na saikolojia ya tiba kutoka Hospitali ya Kinondoni, Adili Kadria anasema nimonia inatokana na hiitilafu zinazotokea katika sehemu moja au mbili za mapafu.
“Inaweza kuwa ni uvimbe ambao husababishwa na bakteria au virusi vinavyoenezwa kwa njia ya hewa na kuifanya mishipa ya kupitisha hewa kushindwa kufanya kazi kutokana na kujaa maji,” anasema Kadria.
Daktari wa Hospitali ya Mkoa wa Geita, Adamu Sijaona anasema nimonia ni ugonjwa unaosababishwa na aina fulani ya seli nyeupe za damu ziitwazo eosinofil ambazo hukusanyika kwenye mapafu.
Dalili
Dk Kadria anasema dalili za awali za nimonia huanza kuonekana ndani ya saa 24 mpaka 48. “Moja ya dalili hizo ni kukohoa. Mgonjwa anaweza kutoa makohozi mazito ya rangi ya njano au kikohozi kikavu,” anasema.
Wataalamu wa afya wanaziweka dalili za nimonia kwenye makundi mawili; za jumla na zile za hatari ambazo mgonjwa anahitaji msaada wa daktari haraka.
Kwa mujibu wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Merland, Marekani, dalili za jumla hutofautiana kulingana na umri. Kwa ujumla wake, dalili hizi huonekana kwa watoto, watu wazima au wazee na zinajumuisha homa inayoambatana na kutetemeka mwili na maumivu ya kifua hasa upande wa pafu lililoumia.
Nyingine ni kikohozi kikavu, kutokwa jasho hasa usiku, kichefuchefu, kutapika na maumivu ya misuli. Mgonjwa pia anaweza kuhisi mapigo ya moyo na pumzi kwenda kasi, kukata pumzi kukichukua muda mrefu kidogo basi uzito unapungua.
Dalili za hatari zinazohitaji huduma za haraka za daktari ni pamoja na homa kali, kushindwa kupumua na rangi ya ngozi kuwa ya bluu. Nyingine ni kikohozi cha makohozi kutoka ndani, kupoteza kumbukumbu hasa kwa wazee, kupungua uzito ndani ya muda mfupi na mapigo ya moyo kwenda kasi.
Aidha, Dk Kadria anasema mgonjwa anaweza kubanwa na kifua, kuhisi maumivu ya kichwa na kupoteza hamu ya kula.
Dk Sijaona anasema: “Watu wanaoshambuliwa zaidi ni wale ambao kinga zao za mwili ni dhaifu. ”
Wataalamu wanasema mgonjwa anahitaji matibabu kwani akiachwa kwa muda mrefu anaweza kusababishiwa kifo. Wanasema vijana wanaweza kupona bila kupatiwa matibabu endapo watakunywa maji mengi.
Kinga
Nimonia unasababishwa na bakteria au virusi na namna ya kwanza ya kuuepuka ni kuzingatia usafi. Mgonjwa anashauriwa kutumia kitambaa kisafi kila anapokohoa au kupiga chafya na kujifuta. Anashauriwa kukitupa kitambaa kilichotumika kwani wadudu wanaweza kukaa humo kwa muda. Vilevile mgonjwa anashauriwa kunawa mikono ili asiwaambukize wengine vimelea vya ugonjwa.
Kulinda afya kwa kuepuka matumizi ya sigara kunakoathiri mapafu na kutoa mwanya wa maambukizi kunasaidia kutoshambuliwa na ugonjwa huo.
Njia ya uhakika ya kukabiliana na nimonia ni chanjo ambayo hutolewa kwa watoto na wazee. Watoto wenye umri chini ya miaka mitano hupewa Pneumococcal Conjugate Vaccine (PCV13) wakati wazee wenye zaidi ya miaka 65 hupewa Pneumococcal Polysaccharide Vaccine (PPSV23).
Tahadhari
Wataalamu wa afya wanansema ugonjwa huu unaotibika endapo muathirika atawahi hospitali na atazingatia ushauri wa daktari. Kupumzika muda wa kutosha na kunywa maji mengi au juisi ya matunda inasaidia kupunguza madhara ya ugonjwa huu.
Mgonjwa asiye na maambuki mengine, inaelezwa kuwa anaweza akapona kwa kuzingatia masuala yaliyobainishwa hapo juu na kujiepusha na mazingira hatarishi. Watu wenye upungufu wa kinga wanashauriwa kukaa mbali na mgonjwa wa nimonia mpaka atakapopona kabisa ili kuepuka maambukizi mapya.
Mikusanyiko ya watu, wataalamu wanabainisha, ni miongoni mwa mazingira rahisi kwa mtu kupata maambukizi hayo. Daktari bingwa wa mapafu wa Hospitali ya Cleveland, Wayne Tsuang alipohojiwa na mtandao wa WebMD juu ya kuanguka kwa Hilary alisema huenda mgombea huyo wa Urais alikuwa walking pneumonia ambayo mgonjwa anakuw ahajitambui kama anayo.
“Inawezekana alikuwa na aina hiyo. Aina hii ya nimonia inasababishwa na bakteria waitwao mycoplasma. Mara nyingi huwashambulia vijana na inaweza ikawepo kwa wiki kadhaa lakini hupona kabla ya kutibiwa. Wengi hupona bila kutibiwa,” alikaririwa Dk Tsuang na kufafanua kuwa ni asilimia 50 ya wagonjwa wa nimonia ndiyo hugundulika ila wanaobaki hutibiwa dalili zake tu.
Source Mwananchi
0 comments:
Post a Comment