728x90 AdSpace

  • Latest News

    Saturday, 24 September 2016

    Utafiti: Kulala mchana kwa zaidi ya saa moja ni chanzo cha kisukari

    By Ephrahim Bahemu, Mwananchi ebahemu@mwananchi.co.tz
    Kusinzia mchana kwa zaidi ya saa moja ni dalili ya kisukari aina ya pili (type 2 diabetes), utafiti unasema. Utafiti huo wa kwanza wa aina yake umefanywa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Tokyo, Japan unabainisha uwekezano huo.

    Watalaamu hao walioongozwa na Dk Yamada Tomahide walipitia tafiti 21 zinazohusianisha kiasi cha usingizi na uwezekano wa kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza; kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na kupooza ambazo zilihusisha watu 307,237 kutoka bara Asia na nchi za magharibi.
    Watafiti hao waligundua kwamba kusinzia kwa muda unozidi dakika 60 kunaongeza hatari ya kupata kisukari aina ya pili kwa asilimia 45 tofauti na kusinzia kusikozidi dakika 40.
    Uchambuzi wa taarifa walizokuwa nazo wataalamu hao, ulidhihirisha kwamba hakuna hatari yoyote kwa mtu anayesinzia mpaka dakika 40 lakini hatari huongezeka ghafla baada ya kuzidi dakika 60.
    “Utafiti wetu umebaini uwepo wa uhusiano wa kusinzia kwa muda mrefu mchana na uwezekano wa kupata kisukari na magonjwa ya kimetaboliki (metabolic syndrome). Utafiti zaidi unahitajika kujiridhisha kuhusu kusinzia kwa muda mfupi,” ilihitimisha ripoti hiyo iliyowasilishwa kwenye mkutano wa 52 wa Shirika la Utafiti wa Kisukari Ulaya (EASD) uliofanyika Munich, Ujerumani mapema mwaka huu.
    Zipo sababu nyingi zinazoweza kuchangia hatari hiyo. Wanasema usingizi mrefu wa mchana unaweza kumaanisha kuwa mtu hakulala vizuri usiku suala linalohusishwa na msongo wa mawazo ambao ni chanzo cha kisukari.
    Akitoa maoni juu ya majibu ya utafiti huo, Profesa Naveed Sattar, daktari bingwa wa magonjwa ya metaboliki kutoka Chuo Kikuu cha Glasgow, Uingereza anasema: “Utafiti huu unaonyesha uhusiano wa kisukari na usingizi mrefu wa mchana. Inawezekana kinachosababisha kisukari ndicho kinaleta usingizi huo. Inawezekana ni sukari imezidi mwilini hivyo usingizi mrefu kuwa dalili ya kisukari.”
    Profesa huyo, akizungumza na mtandao wa WebMD aliendelea kufafanua kwamba: “Baada ya utafiti huu sasa tunao ushahidi kuwa ukosefu wa usingizi wa kutosha usiku kunahusiana na kisukari. Kinachotakiwa ni kufahamu muda gani unahatari hizo kwa afya ya mtu. Tafiti mpya zitatupa majibu ya kina.”
    Watu wengi wana kawaida ya kujipumzisha mchana. Baadhi ya sehemu, kutokana na majukumu, ni ratiba ya siku kwa watendaji wa aina fulani. Usingizi kiasi pamoja na mlo kamili na mazoezi madogo madogo inafahamika kuwa ni misingi ya afya bora ila utafiti huu unatahadharisha kuwa macho na ule uliopitiliza.
    Pamoja na ukweli huo, usingizi wa mchana unapaswa kuwa mfupi, usiozidi dakika 40. Ushauri huu unatolewa ukiwajumuisha pia wafanyakazi wanaoingia kazini usiku kama wauguzi, madaktari, askari na madereva wa magari ya masafa marefu.
    Dezzy Azimio anasema: “Mara nyingi kama sijaenda kazini huwa nalala au inapotokea sina shughuli ya kufanya. Mara chache huwa nahisi usingizi hata nikiwa kazini hasa baada ya kula.”
    Wataalamu
    Daktari wa Hospitali ya Taifa Mhimbili (MNH), John Seka anakubaliana na majibu ya utafiti huo na anasema kuna uhalisia kwani watu wenye kisukari mara nyingi hujisikia uchovu muda mwingi hivyo kulala muda mrefu, mchana na usiku.
    “Inawezekana utafiti huo ukawa na ukweli kwani baadhi ya watu wenye matatizo ya kuchoka mwili ambayo husababisha walale mara kwa mara huwa na hali za kukojoa na kiu ambazo ni dalili za kisukari,” anasema Dk Seka na kuongeza:
    “Wagonjwa wanaokuja hospitali kwa malalamiko ya uchovu wa mwili, wakiulizwa dalili nyingine walizonazo huwa wanazitaja za kisukari na hata ukimpima unakuta tayari ana kisukari aina ya pili.”
    Mtaalamu wa tiba ya kisukari kutoka Hospitali ya Mwananyamala, Dk Nurdin Mavura anasema kuna uhusiano mkubwa na hata madaktari wa nchi nyingine walishafanya utafti huo na kubaini hilo.
    “Mtu anaposinzia kongosho lake huwa halifanyi kazi ya kupunguza au kuongeza sukari wala sukari iliyopo haitumiki mwilini kwa muda. Hivyo basi kama usingizi utakuwa wa muda mrefu ni rahisi kwake kupata kisukari,” anasema Dk Mavura.
    “Watu wanaougua magonjwa yanayowalazimu kulala muda wote nao wapo kwenye hatari ya kupata kisukari kwa kuwa mwili haujishughulishi kuondoa mafuta ya ziada ambayo hutokana na kukaa bila kufanya mazoezi ukija kuwapima unakuta tayari wanaumwa kisukari.”
    Dk Mavura aliongeza kuwa siyo watu wanaosinzia kwa muda mrefu mchana peke yao waliopo kwenye hatari hiyo ya kupata kisukari aina ya pili bali hata wale ambao hukaa muda mwingi au kutembelea sana gari na kukosa muda wa kufanya mazoezi kwa muda mrefu.
    Kifahamu kisukari aina ya pili
    Awali ugonjwa wa kisukari aina ya pili ulijulikana kama aina ya kisukari kisichotegemea insulini au kisukari kinachoanza katika utu uzima.
    Lakini ugonjwa huo ni tatizo la kimetaboliki linalotambulika kutokana na kiwango cha juu cha glukozi katika damu katika muktadha wa kukinza insulini na upungufu wa insulini kwa kiasi kidogo.
    Ugonjwa huu huu ni kinyume na kisukari aina ya kwanza ambacho kinatokana na upungufu wa insulini kufuatia kuharibika kwa seli za endokrini katika kongosho.
    Dalili zake huwa ni kuu ni kiu mara kwa mara, kukojoa kila mara na kuhisi njaa kila wakati.
    Kisukari aina ya pili huchangia hadi asilimia 90 ya visa vya kisukari huku asilimia 10 iliyosalia ikisababishwa na kisukari aina ya kwanza na kisukari katika ujauzito.
    Unene wa kupindukia unaelezwa kuwa ni miongoni mwa sababu zinazochangia kisukari aina ya pili.
    Hata hivyo, wataalamu wanashauri kula chakula kwa kiasi na kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kupunguza hatari iliyopo. Endapo dalili zitajitokeza, mgonjwa anashauriwa kwenda hospitali mara moja ili kupata maelekezo ya kitaalamu kabla hali yake haijawa mbaya.
    Kisukari kinatakiwa kutibiwa mapema ili kuepuka madhara yake. Watalaamu wanaelezwa kwamba kisukari aina ya pili kinaweza kusababisha magonjwa ya moyo, kiharusi, kupungua kwa uwezo wa kuona, matatizo ya figo na kuathiri mzunguko wa damu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Utafiti: Kulala mchana kwa zaidi ya saa moja ni chanzo cha kisukari Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top