Sylvia Mtenga (22), mwanafunzi wa chuo kikuu jijini Dar es Salaam anasema anapenda kuogelea na hufanya hivyo kila anapopata nafasi hasa siku za mwisho wa wiki.
“Mimi na marafiki zangu tunapenda kushindana kuogelea. Tunajisikia vizuri. Hatufanyi hivyo kwa lengo la kujiandaa na michuano ila ni wa afya zetu,” Sylvia.
Watanzania wengi wanapenda kuongelea kutokana na uwepo wa mazingira rafiki ya kufanya hivyo. Wingi wa mabwawa na mito ya asili, maziwa na Bahari ya Hindi ni miongoni mwa vitu vinavyowafanya wengi wauupende mchezo huo kama ilivyo kwa Sylvia.
Fukwe za bahari na maziwa ni miongoni mwa sehemu zinazotembelewa na watu wengi kwa ajili ya burudani hiyo. Hoteli nzuri zimejengwa maeneo hayo kutokana na kivutio hicho kwa lengo la kupata wateja wengi.
Mabwawa ya kuogelea pia yapo kwenye hoteli nyingi zenye hadhi ya juu ambako watoto wakiwa chini ya uangalizi wa familia au walimu hupenda kutembelea na kuogelea. Licha ya matukio kadhaa ya watoto kuathirika na wakati mwingine kupoteza maisha kutokana na kukosa uangalizi makini, maji yana athari sikioni.
Kwa wanaopenda kuogelea ni kawaida maji kuingia sikioni ingawa hutoka baada ya muda. Maji hayo yanaelezwa husababisha maambukizi ya sikio na inashauriwa kuwa makini zaidi ili kuepuka madhara.
Maambukizi ya sikio ni kitu ambacho kila mwogeleaji; mzoefu au anayejifunza anapaswa kuwa makini nayo. Wataalamu wa kuogelea wanasema, mara nyingi, maji huingia sikioni wakati wa anapopiga mbizi au anapozama na kuibuka.
Maji yakiingia sikioni, mhusika anasika maumivu au anapoteza usikivu kwa muda mpaka yatakapotoka. Ushauri unatolewa ili kuepuka jambo hili kwa usalama wa masikio na afya ya waogeleaji.
Mtaalamu
Mtaalamu wa afya kutoka Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili (Muhas), Dk Benjamini Rulakuze anaeleza kuhusu maambukizi ya sikio kwamba yanasababishwa na bakteria au fangasi waishio ndani ya maji.
Anasema mara nyingi maji huwa na bakteria au fangasi na ndiyo maana mabwawa husafishwa mara kwa mara iki kuwaondoa na kuhakikisha afya ya muogeleaji na kumwepusha na maambukizi ya sikio ambayo kitaalamu hujulikana kama Otitis Externa ambayo husababishwa na bakteria waitwao Staphylococcus Aureas au Pseudomanas Auriginosa.
Anasema maji yakiingia sikioni huondoa utando au nta iliyomo ambayo kazi yake kubwa ni kuua bakteria na kunasa na kuutoa uchafu uingiao hivyo kuruhusu bakteria kuishi na kusababisha maamubukizi. Anafafanua kuwa maambikizi haya hayasababishwi na kuogelea pekee bali kuna vitu vingine vinavyochangia mfano matumizi ya pamba za kusafishia masikio (cotton buds) pia huweza huondoa nta hiyo vilevile.
Anazitaja dalili za ugonjwa huu kuwa ni pamoja na sikio kuuma hasa likiguswa sehemu ya nje, kutosikia vizuri na kutokwa uchafu au usaha. Anashauri kila anayeona dalili hizi kupata ushauri wa kitaalamu kabla hali yake haijawa mbaya zaidi na uwezekano wa muleta madhara makubwa.
“Hospitali kuna vifaa maalumu vya kusafishia sikio lenye tatizo kabla dawa zinazohitajika hazijatolewa. Mtu anayechelewa kupata matibabu anaweza kuathirika zaidi na kusababisha maambukizi hayo kupanda hadi kwenye ubongo na kuotesha jipu hatua ambayo ni mbaya na inahitaji upasuaji ili kutibu,” anasema.
Ushauri
Ili kuepuka madhara ya muda mrefu yanayoweza kusababishwa na maambukizi hasa kutokana na maji wataalamu na wadau wa afya wanashauri kila mtu kuwa makini anapoogelea, huku msisitizo ukielekezwa zaidi kwa watoto.
Chama cha Msalaba Mwekundu nchini Marekani kinaeleza masuala muhimu ya kuzingatia kabla na wakati wa kuogelea ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kujitokeza kwa wapenzi wa burudani hiyo.
Usalama wa maisha
Miongoni mwa mambo muhimu kuzingatia wakati wa kuogelea, iwe bwawani, ziwani au baharini usalama ni jambo muhimu. Kila mtu anatakiwa kuogelea kwenye eneo lisilo hatari kwake. Lisiwe lenye kina kirefu kitakachomshinda kujiokoa ikihitajika.
Eneo lenye watoto au waogeleaji wanaojifunza linatakiwa kuwa na usimamizi. Watoto wanapaswa kufundishwa na kuengewa utamaduni wa kuomba watoto kuomba ruhusa kabla ya kwenda kuogelea na kamwe usiwaache peke yao.
Maboya ya kujiokolea
Watoto wadogo na wasiokuwa na ujuzi wa kuogelea wanatakiwa wavae maboya ya kuogelea muda wote wanapokuwa kwenye maji. Licha ya maboya hayo watoto na wanaojifunza kuogelea wanatakiwa kuwa chini ya uangalizi.
Jifunze kuogelea kwa ustadi
Kuogelea ni taaluma na mchezo wenye kanuni za umahiri. Kabla ya kuwa na ujuzi utakaokufanya ufurahie zaidi, inashauriwa kujiunga na madarasa yanayofundisha uogeleaji.
Muda wote wa kufanya hivi inashauriwa kujiepusha na unywaji wa pombe au matumizi ya kilevi cha aina yoyote. Pia, hata baada ya kuwa mahiri kwenye uogeleaji haishauriwi kuogelea ukiwa umelewa.
Usalama wa bwawa
Kwa wanaomiliki mabwawa nyumbani au sehemu nyingine yoyote wanashauriwa kuhakikisha yanakuwa na mipaka ya kina au vizuizi na vifaa sahihi vya msaada na kujiokolea pindi utakapohitajika.
Vifaa hivyo vinaweza kuwa maboya ya kuogelea sanduku la huduma ya kwanza na simu kwa ajili ya mawasiliano ya dharura. Namba za dharura kwa msaada wa haraka zinapaswa ziwekwe sehemu ambayo kila mtumiaji wa bwawa husika ataziona kwa urahisi na kuweza kuzitumia na kupata msaada unaohitajika kwa wakati.
Ulinzi uzingatiwe wakati wote watoto wanapocheza kwenye maji na endapo kuna mmoja kati yao anakosekana au kupungua ni vema akatafutwa haraka kwa kutazama ndani ya maji kwanza kwani sekunde moja inaweza kusababisha kifo au ulemavu kwa watoto.
Tahadhari
Wataalamu wanapendekeza matumizi ya taulo au nguo kukausha sikio baada ya kuogelea badala ya pamba za masikio au vijiti. Wanatahadharisha matumizi ya pamba kwa sababu inaweza kuharibu ngoma ya sikio au kuondoa nta hivyo kuchangia tatizo kubwa kuliko ilivyotarajiwa.
Wataalamu wanashauri kuwa ni vyema kutumia vifaa maalumu vya kuogelea vinavyokinga macho na masikio dhidi ya hatari itokanayo na maji machafu wakati wa kuogelea.
Elimu juu ya magonjwa bado inahimizwa na wataalamu wengi ili watu waweze kujikinga dhidi ya maradhi yanayoweza kuepukika kuliko kusubiri tiba.
Source Mwananchi
0 comments:
Post a Comment