728x90 AdSpace

  • Latest News

    Tuesday 26 July 2016

    Madhara yatokanayo na vipodozi vyenye sumu au feki

    Kwa dunia ya sasa, ni jambo la kawaida sana watu kutumia vipodozi ili waweze kuwa na muonekano wanaotaka!Lakini wimbi la watumiaji limekua likiongezeka siku hadi siku na hii ni kutokana na mabadiliko au mfumo wa maisha ya kisasa..Watumiaji wengi ni akina dada au vijana kati ya miaka 16 hadi 38.Pia kwa miaka ya hivi karibuni kuna wimbi kubwa la vijana walioathirika na utumiaji wa vipodozi visivyo salama na wengi bado hawajui ni vipodozi vipi tunasema ni salama na vingine si salama

    Kutokana na wimbi hili la vijana wengi kuwa na madhara kwa kutokujua au wengine hata kwa kujua, nimeamua kukuletea  makala hii fupi lengo hasa ni kuweza kukusaidia/kuisaidia jamii hii hasa wale wasiofahamu aina za vipodozi vinavyoweza kuleta madhara. Lakini kabla hatujayazungumzia madhara, tuangazie kwa pamoja maana ya kipodozi!

    Nini maana ya vipodozi?

    Sheria ya mamlaka ya chakula, dawa na vipodozi yaani “Tanzania food, drugs and cosmetics act” ya mwaka 2003, inafafanua kuwa kipodozi ni kitu chochote kilichodhamiriwa kutumiwa kwa kupaka, kujimwagia, kujifukisha, kujipulizia au namna nyingine kwenye mwili wabinadamu kwa lengo la kujitakatisha, kujiremba au kuongeza mvuto au kubadilisha muonekano pamoja na mambo mengine yenye malengo kama hayo.

    Ni ukweli usiopingika kuwa vipodozi vimetengenezwa kwa kemikali au viambata ambavyo baadhi si salama na vingine ni salama iwapo vitatumiwa katika mwili wa binadamu.

    Makala hii fupi kama nilivyotangulia kusema itakuwezesha msomaji kujua baadhi ya kemikali zinazoweza kukuletea madhara pindi utakoputumia vipodozi.

    Mamlaka ya chakula na dawa ni mamlaka iliyoanzishwa kisheria na lengo kuu ni kusimamia ubora na usalama wa bidhaa kuanzia zinapotengezwa, kusafirishwa, kusambazwa na kutumiwa na wateja.

     Kutokana na hilo basi, mamlaka hii pia imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti bidhaa ambazo si salama kwa watumiaji hasa vipodozi na dawa feki au zilizokatazwa.

    Tangu kuanza kwa udhibiti, aina 250 za vipodozi zimesha pigwa marufuku kwani zina viambata ambavyo si salama kwa matumizi. Idadi hii inaweza kuongezeka kutokana na matokeo ya chunguzi mbalimbali.

    Mfano wa vipodozi au cream zilizopigwa marufuku ni kama carolite, mikorogo au kama picha hapo inavyoonyesha. Hakika kama unavyoviona ni vipodozi tunavyovijua na wengi bado tukiendeelea kuvitumia.

     Ni viambata vipi au kemikali zipi tunasema si salama?

    Kemikali hizo zinazotajwa ni kama ifuatavyo:

    Biothionol, Hexachlorophene, Zebaki au mercury, Vinyl chloride, zirconium, Halogeneted salicynilides, chloroquinone, steroids, choloroform, methylene chloride na chlorofluorocarbon propellants.

    Madhara

    ·         Kupata mzio wa ngozi na athari kwenye ngozi ikiwa itapata mwanga wa jua kwa

    ·         Baadhi  hupenya kwenye ngozi na kuingia kwenye mishipa ya fahamu na kusababisha ugonjwa wa mishipa ya fahamu hasa kichwa

    ·         kwa wamama wajawazito huweza kuathiri ubongo wa watoto wao

    ·         Ngozi kuwa laini na kusababisha magonjwa kama fangasi au maambukizi ya vimelea vingine

    ·         Zebaki au mercury husababisha madhara ya ngozi, ubongo, figo na viungo mbalimbali.

    ·         Ngozi kuwa laini,mabakabaka, muwasho na mzio wa ngozi.

    ·         Zebaki pia inaweza kusababisha upofu, uziwi, upotevu wa fahamu wa mara kwa mara.

    ·         Kansa

    ·         Kwa viambata vyenye steroids vikitumika kwa muda mrefu husababisha madhara kama ugonjwa wa ngozi na kutokwa na chunusi kubwa, ngozi kuwa nyembamba na laini na endapo mtu atapata jeraha au kufanyiwa upasuaji kidonda hakitapona, pia husababisha magonjwa ya moyo.

    Jitihada za mamlaka ya chakula na dawa

    Mamlaka imejitahidi kwa kiasi kikubwa kupambana na vipodozi hivi feki lakini bado inakabliwa na changamoto kwa mfano wa rasilimali watu, si rahisi wafanyakazi wa mamlaka kuwa kila eneo linalouzwa vipodozi. Pia vipodozi hivi vimekuwa vikiingizwa nchini kupitia katika mipaka isiyo rasmi au njia za panya na walanguzi au wafanya biashara wasio na mapenzi mema kwa afya yako. Pia uelewa wa jamii bado uko chini sana kuhusiana na madhara au matumizi ya viambata vyenye madhara.

    Cha kujifunza

    Hivyo  basi ni jukumu letu sote kama wadau kuweza kusaidiana kuelimisha jamii au kuisadia mamlaka kwa kutoa taarifa za watu wanaovunja sheria za mamlaka kwa kuuza vipodozi vyenye madhara au kemikali tajwa ili waweze kuchukuliwa hatua na hatimaye kuweza kulinda afya za watanzania na taifa kwa ujumla.Pia ni jukumu la watumiaji kuchukua tahadhari kwa kutotumia bidhaa zilizokatazwa na mamlaka kwani ni hatari kwa ustawi wa afya zetu.

    Ni matumaini yangu msomaji umeweza kuzifahamu kemikali zenye madhara,sina la ziada kwa leo na nina amini umeweza kujifunza mengi kuhusiana na madhara yatokanayo na viambata vyenye sumu kwenye vipodozi.

    Imeandaliwa na  Mfamasia, Michael Bajile.

    18th January 2015

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Post a Comment

    Item Reviewed: Madhara yatokanayo na vipodozi vyenye sumu au feki Rating: 5 Reviewed By: Unknown
    Scroll to Top